Judges 18:7-27

7 aBasi hao watu watano wakaondoka na kufika Laishi, mahali ambapo waliwakuta watu wanaishi salama, kama Wasidoni, kwa utulivu na bila mashaka. Nchi yao haikupungukiwa na kitu chochote, hivyo wakawa tajiri. Pia walikaa mbali sana na Wasidoni, wala hawakushughulika na mtu yeyote.

8Waliporudi kwa ndugu zao huko Sora na Eshtaoli, ndugu zao wakawauliza, “Mlionaje mambo huko?”

9 bWakajibu, “Twendeni, tukapigane nao! Tumeona kuwa nchi ni nzuri sana. Je, hamtafanya chochote? Msisite kupanda ili kuimiliki. 10 cMtakapokwenda huko mtakuta watu waliotulia walio salama, nayo nchi hiyo ni kubwa na Mungu ameitia mikononi mwenu, nayo ni nchi ambayo haikupungukiwa na kitu chochote kilicho duniani.”

11 dNdipo watu 600 toka ukoo wa Wadani, waliojifunga silaha za vita, wakaondoka Sora na Eshtaoli. 12 eWalipokuwa wakisafiri wakapiga kambi huko Kiriath-Yearimu katika Yuda. Hii ndiyo sababu sehemu ya magharibi ya Kiriath-Yearimu inaitwa Mahane-Dani
Mahane-Dani maana yake Kambi ya Dani.
mpaka leo.
13 gKutoka hapo wakaendelea mbele mpaka nchi ya vilima ya Efraimu na kufika katika nyumba ya Mika.

14 hNdipo wale watu watano waliopeleleza nchi ya Laishi wakawaambia ndugu zao, “Je, mwajua kuwa mojawapo ya nyumba hizi kuna naivera, sanamu ndogo za nyumbani, sanamu ya kuchonga na sanamu ya kusubu? Sasa basi fikirini mtakalofanya.” 15Basi wakaingia humo na kwenda kwenye nyumba ya yule kijana Mlawi katika nyumba ya Mika na kumsalimu. 16Wale Wadani 600, waliovaa silaha za vita, wakasimama penye ingilio la lango. 17 iWale watu watano waliokwenda kupeleleza nchi wakaingia ndani na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani pamoja na ile sanamu ya kusubu, wakati yule kuhani akiwa amesimama pale penye ingilio la lango pamoja na wale watu 600 waliokuwa wamejifunga silaha za vita.

18 jHao watu walipoingia katika nyumba ya Mika na kuchukua ile sanamu ya kuchonga, ile naivera, na zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, pamoja na ile sanamu ya kusubu, yule kuhani akawauliza, “Mnafanya nini?”

19 kWakamjibu, “Nyamaza kimya! Weka mkono wako juu ya kinywa chako na ufuatane nasi, uwe baba yetu na kuhani wetu. Si ni afadhali utumikie kabila na ukoo katika Israeli kama kuhani kuliko kumtumikia mtu mmoja na watu wa nyumbani mwake?” 20Yule kuhani akafurahi. Akachukua ile naivera, zile sanamu nyingine ndogo za nyumbani, na sanamu ya kuchonga, naye akaenda pamoja na wale watu. 21Ndipo wakageuka na kuondoka wakiwatanguliza mbele watoto wao wadogo, wanyama wao wa kufugwa na mali zao.

22Walipokuwa wamesafiri umbali kidogo toka nyumbani kwa Mika, watu walioishi karibu na Mika wakaitwa wakakusanyika pamoja, nao wakawafikia Wadani. 23Walipofuatilia wakipiga kelele Wadani wakawageukia na kumwambia Mika, “Una nini wewe hata ukaja na kundi la watu namna hii ili kupigana?”

24Akawajibu, “Mmechukua miungu yote niliyoitengeneza, mkachukua na kuhani wangu, nanyi mkaondoka. Nimebaki na nini kingine? Mnawezaje kuniuliza, ‘Una nini wewe?’ ”

25Wadani wakamjibu, “Usibishane na sisi, la sivyo watu wenye hasira kali watakushambulia, nawe na watu wa nyumbani mwako mtapoteza maisha.” 26 lBasi Wadani wakaenda zao, naye Mika alipoona kuwa wana nguvu kumliko yeye, akageuka na kurudi nyumbani kwake.

27 mKisha wakachukua vile Mika alivyokuwa ametengeneza, na kuhani wake, wakaendelea hadi Laishi, dhidi ya watu walio na amani, wasiokuwa na wasiwasi. Wakawashambulia kwa upanga na kuuteketeza mji wao kwa moto.
Copyright information for SwhNEN